Hotuba ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Baraza la Eid-el-Fitr, Arusha, tarehe 24 Oktoba, 2006

 

Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba;

Mhe. Mkuu wa Mkoa,

Mheshimiwa Mbunge wa Arusha;

Mheshimiwa Naibu Mufti, Sheikh Abubakar Zubeir;

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;

Wajube wa Baraza Ulamaa;

Waheshimiwa Masheikh na Viongozi wa BAKWATA;

Mheshimiwa Baba Askofu Laissor,

Waheshimiwa Viongozi wa Dini na Madhehebu Mbalimbali;

Viongozi wenzangu wa Chama na Serikali;

Ndugu wananchi;

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana;

Assalaam Eleykum warahmattullah taallah wa-Barakatuh!

Eid-Mubarak!

Naungana na Masheikh walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai na kutuwezesha kushiriki katika Baraza la Idd la mwaka huu.

Nakushukuru sana Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Issa bin Shaaban Simba kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kuadhimisha kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mmenipa heshima kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Eid mwaka huu. Najiona kuwa mtu mwenye bahati kwa kupewa heshima kubwa kama hii kwani kama mjuavyo, mimi siyo Sheikh na wala si mwanazuoni. Ni Muislam wa kawaida kabisa. Hivyo basi, kila ninapoalikwa kuzungumza katika shughuli kama hizi hugwaya kuhusu nini cha kuwaambia watu mabingwa katika mambo ya dini kama mlivyo nyie. Lakini kwa vile mmejiaminisha kuwa naweza kufaa, nami nimejiaminisha hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mufti;

Niruhusu nianze kwa kuwapongezaWaislamu wenzangu wote nchini na duniani kwa kumaliza salama mfungo wa mwaka huu wa mwezi wa Ramadhani. Naungana nanyi na Waislamu wenzangu nchini na duniani kote kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhana Wa-taala, kwa kutujalia baraka zake na kutuwezesha kufunga na kumaliza salama. Tuzidi kumuomba Manani atupe uzima na afya njema ili tuuone mfungo wa mwaka ujao na tufunge na kumaliza salama kama ilivyokuwa mwaka huu.

Mheshimiwa Sheikh Mkuu naNdugu zangu Waislamu;

Mimi binafsi na wenzangu wote Serikalini tunatambua kwamba mfungo wa mwaka huu umefanyika katika mazingira magumu kidogo kutokana kuwepo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa umeme nchini. Nafahamu vyema kwamba ukosefu wa umeme umewakarahisha Waislam wengi hasa pale ulipokosekana wakati wa sala au wakati wa kuandaa futari au daku.

Ndugu Zangu;

Tatizo la ukosefu wa umeme hapa nchini ni tatizo linalotusikitisha na wakati mwingine linalotusononesha sana. Tunaomba radhi kwa usumbufu mlioupata kama vile ambavyo tunawataka radhi Watanzania wengine wote kwa usumbufu wanaoupata kutokana na tatizo hili la umeme. Ni tatizo la Watanzania wote na wala halikubagua Misikiti au Waislamu pekee. Napenda kuwahakikishia kwamba kiini cha tatizo si uzembe wa mtu yoyote bali ni mitihani ya Mwenyezi Mungu kutokutupatia mvua za kutosha na hivyo kusababisha mabwawa yetu ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu kutopata maji ya kutosha kuzalisha umeme wakati wote wa mwaka.

Bahati mbaya sana kwa upande wa tatizo la umeme hakuna majawabu ya papo kwa papo. Hata kwa umeme wa dharura imetuchukua miezi isiyopungua mitano tangu tuanze mchakato wa kukodi mitambo ya kuzalisha umeme. Ni sasa tu ndipo baadhi ya mitambo imewasili na baadhi kuanza kazi. Ni matumaini yetu kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao au hata katikati karibu mitambo yote ya kukodi itakuwa imewasili na kuanza kuzalisha umeme. Mitambo hii itakapoanza kuzalisha umeme, tutakuwa tumepata nafuu. Lakini, jawabu hasa litakuwa limepatikana hapo mwakani wakati mitambo mipya ya TANESCO ya Ubungo na Tegeta itakapokuwa imeanza kutoa umeme.

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh na Ndugu Wananchi;

Nawasihi Watanzania wenzangu tuendelee kuwa wavumilivu na wenye moyo wa subira wakati Serikali inaendelea kukabiliana na tatizo hili. Naelewa hisia ya mtu mwenye tatizo kubwa anayesubiri jawabu la haraka kila unapomwambia awe na subira anaona humpatilizi. Napenda kuwahakikishia tena kuwa tatizo hili tunalitambua, linatugusa sote, linatusikitisha na kutusononesha sana. Tunalifuatilia kwa karibu sana na wakati mwingine hukesha tukihangaikia utatuzi wake.

Mheshimiwa Mufti;

Ni makusudio yetu kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hili na hatua tunaendelea kuchukua. Bahati mbaya, kama nilivyokwishasema, tatizo hili halina majawabu ya haraka haraka. Halifanani na lile la njaa ambapo ukiwa nazo pesa unalipa na kupewa magunia yako ya mahindi au mchele wakati huo huo na kuyasafirisha. Kwa umeme lazima usubiri. Hakuna mitambo inayosubiri mnunuzi dukani.  Ni lazima itengenezwe kama unataka mipya na hata kama utanunua au kukodi uliotumika lazima usubiri ufunguliwe hapo ulipofungwa kabla ya kupakiwa tena na kuletwa kwako.

Kwa ujumla, naridhika na jitihada zinazofanywa na viongozi na watendaji wetu Serikalini na mashirika yake husika katika kukabiliana na tatizo hili. Kumekuwepo na ulegevu na makosa ya hapa na pale ambayo tumekuwa tunachukua hatua kila tulipoyabaini na hatutasita kuchukua hatua zaidi kama hapana budi. Nia yetu ni kuwahudumia Watanzania. Tutafanya kila tuwezalo wajibu wetu huo tuutimize ipasavyo.

Dini na Amani, Utulivu na Mshikamano

Mheshimiwa Mufti,

Uhuru wa kuabudu ni moja ya haki za msingi za kila mwananchi wa Tanzania. Kila Mtanzania anao uhuru wa kuabudu dini anayoiamini au kuipenda. Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba uhuru huo unaheshimiwa na kuonekana kuwa unaheshimiwa. Ni msingi muhimu uliojenga umoja, amani na mshikamano wa wananchi wa Tanzania na wa nchi yetu kwa jumla, tangu uhuru mpaka sasa. Serikali zetu zote zilizopita ziliheshimu na kuzingatia haki hiyo na hata sasa tutafanya hivyo hivyo. Hatutafanya pungufu ya hapo.

Mheshimiwa Sheikh Mkuu;

Tunatambua kuwepo kwa watu wachache au vikundi vichache vya watu katika jamii wanaopenda kuchochea uhasama na kutokuelewana kati ya Waislam na Wakristo au kati ya taasisi na madhehebu tofauti ya Wakristo na Waislam. Wakati mwingine wanafanya hivyo hata ndani ya dini au madhehebu mamoja. Nataka kuwahakikishia kwa mara nyingine tena Watanzania wenzangu kuwa Serikali haitawaachia hawa watu wakorofi au waovu wachache waivuruge nchi yetu. Wakati wote tutakuwa macho na makini kuhakikisha kuwa hawapati fursa ya kufanya uovu wao. Tumefanikiwa miaka yote huko nyuma, hatuwezi kushindwa sasa.

Mheshimiwa Mufti na Ndugu Wananchi;

Napenda kuitumia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Watanzania wenzangu kwa kuiletea heshima na sifa kubwa nchi yetu. Hatuna budi kuidumisha na kuiendeleza sifa hii. Nawapongeza kwa namna ya kipekee viongozi wa siasa wa nchi yetu kwa kuitikia wito wa kuepuka udini katika shughuli za kisiasa. Kadhalika, natoa pongezi kwa viongozi wa dini kwa kutochochea ubaguzi na uhasama miongoni mwa Watanzania kwa misingi ya dini zao.

Nchi yetu imeendelea kuwa ya amani kwa sababu ninyi viongozi wa dini mmehubiri amani kwa waumini wenu; na, nchi yetu imeendelea kuwa yenye umoja na mshikamano kwa sababu hamkutoa mawaidha na mahubiri ya kueneza chuki, utengano na mifarakano. Nyote nawashukuru, nawapongeza na kuwasihi mshikilie msimamo huo. Nawaomba pia muwahimize wale wachache miongoni mwenu walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki dhidi ya dini na waumini wa dini nyingine, waache kufanya hivyo.  Ni vyema sote tujue kuwa katika mifarakano na hasama za kidini hakuna atakayeibuka mshindi bali wote tatakuwa ni watu tulioshindwa.

Ni muhimu sote tukatambua haki ya kuwepo kwa watu wa dini na imani tofauti katika jamii zetu. Watu hao wapo na wataendelea kuwepo daima. Ni muhimu, pia kutambua haki ya kikatiba na utashi wa kibinadamu, ambao unalindwa pia na Katiba yetu, ya watu kufuata dini na imani wazitakazo. Totauti za dini na imani hazina namna ya kutokuwepo. La msingi ni kuukubali ukweli huo na kukubali kuishi na wenzako wa dini tofauti na yako. Hili linawezekana kwani ndivyo ilivyo hivi sasa hapa kwetu.

Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania;

Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kwamba Serikali yetu kamwe haitarudi nyuma kuhusu kuheshimu uhuru wa raia wa kuabudu na kuhubiri dini, ila wasichochee chuki na uhasama miongoni mwa wafuasi wa dini nyingine au madhehebu mengine. Kufanya kinyume chake ni kuvunja sheria za nchi. Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kulinda amani bila woga, huba au upendeleo. Watu wa aina hiyo hatutakuwa na ajizi nao.

Mimi na wenzangu Serikalini hatuna masihara na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi yetu. Wakati wote tutakuwa wakali na wepesi kuchukua hatua. Msichelee kutuarifu mnapobaini vitendo vya kuvuruga amani na mshikamano wa watu wa nchi yetu misikitini, makanisani, kwenye mahekalu, mitaani au kwenye mihadhara.

Mchango wa Dini katika Kuleta Maendeleo

Mheshimiwa Mufti, Ndugu Waumini;

Wakati wote nilipopata fursa ya kuzungumza na viongozi wa dini sikuacha kutambua mchango mkubwa unaotolewa na viongozi na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali ya dini nchini. Na, leo nataka kufanya hivyo hivyo. Mmesaidia sana kueneza huduma za jamii, hasa afya, elimu na nyinginezo ambazo zimesaidia katika kuleta maendeleo ya Taifa letu kwa jumla. Mchango na juhudi hizi ni za muda mrefu, kuanzia kabla ya uhuru wa nchi yetu mpaka sasa.

Kwa kweli sasa umekuwa kama ni utamaduni uliojenga matumaini kwa Watanzania juu ya mchango na nafasi ya mashirika ya kidini katika kuendeleza na kuboresha maisha yao, siyo tu ya kiroho bali hata ya kimwili na kuwaletea maendeleo. Napendezwa sana na jitihada hizi na ningependa ziendelezwe na kupanuliwa zaidi. Nawahakikishia ushirikiano wa Serikali na hata msaada kama hapana budi ili malengo yenu yatimie.

Mheshimiwa Mufti;

Nimefurahi sana kusikia kwenye salamu zenu mlizotoa hivi punde kwamba BAKWATA nayo imepania kuendeleza juhudi kubwa za kueneza na kutoa huduma za jamii, hasa za afya na elimu, kwa Watanzania. Pia mmefikiria kuwa na mipango ya kuwasaidia waumini wenu wajiendeleze kiuchumi. Nimefarijika sana kuona muelekeo na msisitizo huu mpya kwani ni ukweli usiofichika kwamba mchango wa mashirika ya dini ya Waislamu hasa wa Suni, ambao ndiyo wengi hapa nchini, siyo mkubwa sana katika maeneo ya elimu na afya ukilinganisha na wenzetu wa dini nyingine au hata madhehebu mengine. Naamini, kwa mwamko huu mpya na kama mtajipanga vizuri katika Baraza na kutoa uongozi thabiti inawezekana kabisa kwa Waislamu nao kutoa mchango mkubwa wa kuonekana.

Naamini hivyo kwa vile pamoja na ukweli kwamba Waislamu wengi ni maskini lakini wapo wachache ambao ni matajiri na wengine ni matajiri wakubwa ambao wanaweza kuwa watu wa msaada mkubwa. Kadhalika, yapo mataifa kadhaa ya Kiislamu na wapo Waislamu duniani ambao ni matajiri na hutoa zaka kila mwaka kusaidia mambo kama hayo ya huruma. Naamini wakiombwa wanaweza kusaidia. Lakini, hapa nchini na hata duniani wapo watu wasiokuwa Waislamu ambao huchangia sana maendeleo ya wanadamu wenzao bila kubagua kwa dini zao au rangi zao. Nao pia wakiombwa, naamini watachangia juhudi za BAKWATA na wakati mwingine wanaweza kuchangia hata kuliko waislamu matajiri kwani kutoa ni moyo si utajiri.

Mheshimiwa Mufti;

Waheshimiwa Masheikh;

Kinachotakiwa ni uongozi thabiti na ufuatiliaji wa dhati na makini wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania wakiongozwa na wewe mwenyewe Mufti wetu. Kwanza kabisa Baraza liwe na muelekeo ulio wazi wa kisera unaotoa kipaumbele stahiki kwa masuala ya kuendeleza elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa wanadamu kama vile maji na kadhalika. Pili, pawepo na mikakati na programu za utekelezaji wa mipango hiyo. Tatu, pawepo na utaratibu au mfumo maalum wa uendeshaji wa kuongoza na kusimamia utekelezaji wa programu na miradi ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Nadhani kwa miaka mingi huko nyuma mambo haya matatu ya msingi yamekuwa pungufu katika chombo chetu hiki muhimu ndiyo maana hatukupiga hatua kubwa ya maendeleo katika maeneo haya. Lakini, pia sifa ya Baraza letu haikuwa nzuri sana kwa upande wa usimamizi na udhibiti wa fedha na mali za Baraza. Uaminifu wa uongozi na watendaji wa Baraza umekuwa unatiliwa mashaka kiasi cha kuwafanya watu wengi wenye uwezo kuchelea kuchangia kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania. Matokeo yake ni kukosekana kwa misaada muhimu kutoka kwa watu wenye nia njema nchini na hata kwingineko duniani. Wapo waliochangia kupitia kwa baadhi ya watu waliowaamini au kuwafahamu. Aghalabu hata njia hiyo haikuzaa matunda yaliyotarajiwa.

Hivyo basi, Mheshimiwa Mufti na Waheshimiwa Viongozi wa Baraza, kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa fedha na mali za Baraza na kuwa na uaminifu katika usimamizi na matumizi ya fedha na mali za Baraza ni jambo la nne la msingi. Lazima Baraza Kuu la Waislamu Tanzania liwe nayo sifa hiyo na lazima ionekane kuwa ipo ndipo mtakapofanikiwa kupata michango mingi ya kufanya shughuli hizi muhimu mnazokusudia kufanya. Lazima pawepo na kuaminiwa na kuaminika ndipo mfanikiwe. Sina shaka, kwamba hii inawezekana ila kuwepo dhamira ya dhati ya kuwa hivyo.

Na, Tano, pawepo na mshikamano na umoja miongoni mwa Waislamu. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Waislamu wanahitaji kuwa na mshikamano ndipo waweze kukabili matatizo lukuki yanayawakabili hasa yale ya kuondoka katika hali ya kuwa nyuma kwa maendeleo. Lakini, muda tunaoutumia kugombana ni mwingi. Tuache. Tubadilike.

Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania;

Nakupongeza sana kwa kuanzisha Mfuko wa Mufti wa Elimu na Maendeleo. Nimefurahi sana kusikia kwamba, toka uzinduliwe mwaka jana. Mfuko huu tayari umekwishasaidia wanafunzi 120, wakiwemo yatima na wasiojiweza, kwa mafunzo ya Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu.  Ndugu zangu tukiwekeza katika elimu hatupotezi bali tunawekeza katika hatima nzuri ya uhakika ya watoto wetu.

Nawapongeza wote waliouchangia na nawaomba wale ambao bado hawajafanya hivyo basi nao wasaidie. Napenda kuitumia nafasi hii kumpongeza kwa dhati Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa kwa mchango wake mkubwa wa shillingi milioni 20 kwa Mfuko wa Elimu wa Mufti. Maadamu mzee ameonyesha njia na mimi nimehamasika kufuata nyayo, nitajipapasa na kutoa mchango wangu kwa kiasi nitakachojaaliwa.

Waislam Kujiimarisha Kiuongozi na Kitaasisi

Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania;

Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;

Dhamira yenu ya kuongeza mchango wa BAKWATA au wa Taasisi za Kiislam katika kutoa huduma za jamii na kuleta maendeleo itatimia tu iwapo tutakuwa na uongozi imara wa Waislam na taasisi za dini ya Kiislam zinazoendeshwa vizuri.

Nawashukuru kwamba katika salamu zenu mmeonesha nia ya BAKWATA ya kujiweka sawa kuchukua nafasi yake stahiki na kutimiza ipasavyo wajibu wake kwa Waislamu na kwa jamii nzima ya Watanzania. BAKWATA ndicho chombo kikuu cha uongozi wa Waislamu na tungependa kuona BAKWATA inaaminiwa na kuheshimiwa na Waislam wote nchini. BAKWATA ndicho chombo kikuu kinachotegemewa cha kuwaunganisha na kuwaongoza Waislamu katika kuendeleza maslahi yao ya kiimani na kimaendeleo. BAKWATA haina budi iwe ndilo kimbilio la Waislam kwa matatizo yao ya kiroho na kimwili.

Mheshimiwa Mufti,

Hii ina maana kwamba lazima BAKWATA ijihusishe na ionekane kuwa karibu zaidi na maisha ya Waislamu kwa mambo yahusuyo dini yao, yaani Uislamu wao na kwa mambo yahusuyo maisha yao ya kidunia yaani maendeleo yao. Kwa upande wa maisha ya kiimani ya Waislamu BAKWATA inao wajibu wa kuwa chombo kikuu cha maongozi ya uenezaji na uendelezaji wa dini ya Kiislamu.

BAKWATA iwe ndipo mahali pa Waislamu kwenda wanapotaka vitabu vya dini: majuzuu, misahafu na vitabu mbalimbali vya elimu ya dini ya Kiislamu. Baraza liwe na maduka ya vitabu, na ijishughulishe na uchapishaji wa vitabu na maandiko ya dini. Ikiwezekana Baraza liwe na mitambo yake ya kuchapisha vitabu na maandiko mbalimbali ya dini. Baraza liwe chombo cha kuhimiza na kusaidia wanazuoni kuandika vitabu na makala za mambo ya kidini. Liwe chombo cha juu kabisa ambacho ndicho kimbilio la wanazuoni na waumini kupata ufumbuzi au ufafanuzi wa masuala ya kidini yanayowatatiza.

Mheshimiwa Mufti;

Nimepata faraja kubwa sana niliposikia kwenye salamu zenu kuwa mnautambua vyema wajibu wenu huo na kwamba mmeainisha vizuri jinsi gani mmepanga kuutimiza. Kwangu mimi, salamu zenu zinaashiria kuzinduka au hata naweza kusema kuzaliwa upya kwa chombo chetu hiki muhimu cha Waislamu yaani Baraza Kuu la Waislamu Tanzania. Ninawahimiza na kuwasihi kuyazingatia mliyoamua kufanya na muhakikishe kuwa mnafanya. Mimi naamini kuwa mambo yote mliyodhamiria kufanya yanatekelezeka kinachotakiwa ni nyie wenyewe katika BAKWATA kuweka mikakati mizuri ya utekelezaji na kuwa makini katika ufuatiliaji wake.

Kama mambo yakiwa hivyo Waislamu watafurahi na kuridhika na chombo chao. Kwa hali hiyo viongozi wa BAKWATA siyo tu watakuwa na madaraka ndani ya BAKWATA bali pia watakuwa na mamlaka mbele ya Waislamu na kwa shughuli za Uislamu hapa nchini.

Mheshimiwa Mufti;

Waislamu wa Tanzania wanahitaji na wanastahili kuwa na chombo imara cha kuwaunganisha na kuwapatia fursa ya kuzungumzia na kuendesha mambo yahusuyo maslahi yao ya kiroho na kimwili. Wanapokosa chombo hicho, Waislaimu wanakosa umoja, wanakosa mshikamano na huwa wanayumba au kuyumbishwa sana. Wakati mwingine katika kubabaika kwao huko baadhi huangukia katika mikono ya watu wabaya na wakatumika kwa mambo yasiyokuwa na maslahi kwa Waislamu wala Uislamu au Taifa kwa jumla. BAKWATA inao wajibu wa kuondoa kasoro hiyo.

Mheshimiwa Mufti na Waheshimiwa Viongozi;

Kama mjuavyo taratibu za uongozi na uendeshaji wa shughuli za dini ya Kiislamu hasa ya dhehebu la Suni tofauti na zile za dini ya Kikristo na hata za madhehebu mengine ya dini ya Kiislamu. Wenzetu wana uongozi unaoanzia chini mpaka juu kitaifa na hata kimataifa. Ni utaratibu uliokuwepo tangu enzi na enzi. Wakristo wana Paroko au Mchungaji kiongozi wa kanisa. Wana Jimbo linaloongozwa na Askofu, wana Jimbo Kuu linaloongozwa na Askofu Mkuu na wana Mkuu wa Kanisa kwa nchi na wana uongozi wa Kimataifa. Wenzetu Bohora, Ismailia na hata Shia wako karibu hivyo hivyo. Wahindu nao karibu sawa.

Kwa upande wetu kimsingi uongozi huanzia na kuishia msikitini na wala hakuna msikiti mkubwa wenye mamlaka kwa mdogo. Kadhalika hakuna Sheikh mkubwa mwenye mamlaka ya amri kwa wenzake. Ni dini iliyojengeka kwenye msingi wa usawa wa waumini na misikiti yao. Katika mazingira hayo kuwepo chombo cha kuwaunganisha Waislamu baada ya ngazi ya misikiti ni jambo jema na la manufaa ya aina yake.

Nawapongeza viongozi waliobuni wazo la kuwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania. Ni wazo zuri na la manufaa sana. Kilichobakia sasa ni kwenu viongozi wa BAKWATA kutambua umuhimu na unyeti wa chombo hicho na kuishi na kufanya kazi kwa shabaha na malengo yake. Lazima wakati wote mtambue hayo na kufanya kazi kwa moyo wa kujituma kwa maslahi ya Waislamu na ya Watanzania wote kwa jumla.

Nimefarijika sana nilipoambiwa kwamba BAKWATA imeanza kuchukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuitazama upya Katiba yake kwa nia ya kuirekebisha na kuleta ufanisi zaidi katika uendeshaji wa shughuli zake. Ni kitendo cha maendeleo endeleeni kufanya hivyo.

Mapambano Dhidi ya Ukimwi

Mheshimiwa Mufti;

Nimefurahi sana pia kusikia kwamba BAKWATA nayo inajihusisha na mapambano dhidi ya UKIMWI. Mnatoa huduma za afya na ushauri nasaha kwa walioathirika na UKIMWI. Hili ni jambo la kutia moyo sana. Nawasihi muendelee nalo kwa nguvu zaidi.

Pamoja na hayo nawaomba muelekeze nguvu kubwa katika juhudi za kuzuia maambukizi mapya ili kuwanusuru waumini wengi na Watanzania wengi ambao wako salama wasiambukizwe. Tunaweza kabisa kudhibiti maambukizo kama viongozi wa dini wataendelea kuwashawishi na kuwahimiza waumini wao kujiepusha na UKIMWI. Ugonjwa huu unaweza kuepukika kama waumini watawasikiliza viongozi wao wa dini na kuzingatia mafundisho yao. Kwa hiyo nawaomba viongozi wa dini muendelee kuhimiza waumini wenu wazingatie mahubiri yenu. Kwa ajili hiyo, nawaomba mfanye mambo matatu. Mosi, muendelee kuwanasihi waumini wenu waepukane na zinaa. Ukweli ni kwamba hii ndiyo njia kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huu. Hivyo basi watu wakiepuka zinaa kama inavyoelekezwa na Mwenyezi Mungu, S.W. ugonjwa huu unaepukika. Pili, naomba muwahimize waumini wenu wawe na subira hasa wale wasiokuwa na ndoa na kuwahimiza wangoje hadi watakapooa au kuolewa.

Na, tatu nawaomba mzidi kuwakumbusha na kuwahimiza waumini wenu waliooa au kuolewa wawe waaminifu kwa ndoa zao. Waridhike na wenzi wao waache kuruka ruka. Wahenga wamesema ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu.

Mheshimiwa Mufti;

Kwa bahati nzuri mambo haya ninayoyasisitiza ndiyo mnayowahubiria waumini wenu kila mara wafanye katika maisha yao kama waumini. Nawaomba muendelee kufanya hivyo kwa nguvu zenu zote kila wakati bila kuchoka. Hali ya maambukizi nchini ni mbaya, naomba tutambue hivyo na tujitokeze sote kwa hali na mali kupambana na maradhi haya. Lazima tushinde katika vita hivi kwani tukishindwa taifa litakuwa limeangamia.

Hitimisho

Mheshimiwa Sheikh Mkuu;

Ndugu Wananchi;

Naomba nimalize kama nilivyoanza kwa kusema kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa uhuru wa Watanzania wa kuabudu unaheshimiwa. Wananchi wataendelea kuwa na uhuru wa kuendesha mambo yao ya dini kwa kadri wanavyoona inafaa, bila ya kuingiliwa ili mradi hawavunji sheria za nchi.

Katika kufanya hivyo tunaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, ambayo mimi na Viongozi wenzangu Serikalini tumeapa kuilinda, kuitunza na kuitetea. Naomba ninukuu kifungu cha 19 cha Katiba:

“(i) Kila mtu anastahiki kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake. Na, (ii) Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi”

Naomba sote, tuhakikishe kuwa matakwa haya ya Katiba ya nchi yetu tunayalinda na kuyatekeleza. Tukifanikiwa kufanya hivyo, naamini nchi yetu itaendelea kuwa ya watu wanaoishi pamoja kwa upendo, amani na utulivu licha ya tofauti zao za imani.

Mheshimiwa Mufti;

Serikali yetu imefikisha miezi kumi sasa tangu ianze kazi ya kuwatumikia Watanzania. Bado tunayo safari ndefu sana katika kutimiza yale tuliyoyakusudia na tuliyowaahidi Watanzania. Naomba niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwatumikia kwa nguvu zetu zote na kwa kutumia vipaji vyote tulivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu bado tunayo. Sababu tunayo na uwezo tunao kwani mamlaka mmetukabidhi.

Naomba niitumie fursa hii kuwashukuru viongozi na waumini wa dini zote nchini kwa kuendelea kuiombea Serikali yetu na sisi viongozi wake ili tutimize vyema wajibu wetu na tufanikiwe katika malengo yetu ya maendeleo tuliyojiwekea. Nawashukuru zaidi kwa kuiombea nchi yetu iendelee kuwa ya amani, utulivu na yenye maendeleo. Kwa hakika mimi, Serikali yetu na nchi yetu tunahitaji na tunastahili kuombewa dua njema ili mambo yaende vyema, tutekeleze malengo tuliyojiwekea kwa manufaa yetu sote. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuyafanya magumu kuwa mepesi. Tuendelee kumuomba.

Binafsi, najisikia kuwa mtu mwenye bahati kubwa kupata nafasi ya kuliongoza taifa lenye wacha Mungu wengi na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali. Watu wenye nia njema na mapenzi kwa Serikali yao na nchi yao na wako tayari kuiombea. Inanipa hamasa na moyo wa kuwatumikia kwa ari, nguvu na kasi kabisa.

Nitaendelea kutegemea dua, ushirikiano, ushauri na msaada wa viongozi na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali nchini katika kuliongoza taifa letu na kulivusha kuelekea kule tunakotarajia sote tuende na tufike salama.

Mwisho kabisa nakushukuru tena, Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunipa heshima hii kubwa. Nawatakia Waislam wote na Watanzania wote kwa jumla sherehe yenye furaha na faraja tele. Tuisheherekee kwa amani na utulivu.

Hija: Mimi nitawagharamia watu watano.

 

Mungu Ibariki Afrika

   Mungu Ibariki Tanzania

  Eid Mubarak!   

Assalam Aleykum Warahmatullahi Taala, Wabarakatuh.

Asanteni Sana kwa kunisikiliza!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s