TAMKO LA WAISLAMU JUU YA MAHAKAMA YA KADHI

Nukta za Kuzingatiwa katika Tafakari ya mwenendo wa wa suala la Mahakama ya Kadhi.

Tarehe 29/Juni/2010, Mufti wa Bakwata alinukuliwa na TBC1 akisema Mahakama ya Kadhi itaanzishwa na kilichobaki ni namna ya uanzishwaji wake na taratibu zake tu.

 

Awali ya hapo, tarehe 25/Juni/2010, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Bw. Pius Msekwa alinukuliwa na TBC1 akisema kwamba serikali ya CCM haitounda Mahakama ya Kadhi kwani ni kinyume na Katiba na kwamba Mahakama hiyo itaundwa na waislamu wenyewe na tayari waislamu wanaendelea na mchakato huo wakiongozwa na Sheikh Mkuu.

 

Kauli ya Mhe. Msekwa si ngeni kwetu. Tunapaswa kutahadhari na kauli hizi kwa sababu zinaashiria hali si nzuri kinyume na Mufti wa Bakwata anavyoeleza au anavyotaka waislamu tuamini.

 

Hii ni kwa sababu, baada ya kuundwa jopo la masheikh, tuliandaa muswaada wa Mahakama ya Kadhi tunayoihitaji, tukaupitia na kisha uwasilishwa katika kikao cha pamoja cha jopo la masheikh kati ya Hay-at na Bakwata ukajadiliwa na ukapitishwa kisha ukawasilishwa kwa Mhe. Waziri Mkuu siku aliyokutana na jopo la masheikh.

 

Kwa hiyo kipimo chetu kuhusu mazungumzo kati ya Kamati teule ya Mufti wa Bakwata na serikali kinapaswa kuwa je, serikali imekubali mapendekezo ya waislamu ama laa na kama imeyakubali ni kwa kiasi gani?

 

Kipimo chochote kingine ni kwenda kinyume na msimamo wetu wenyewe na kukubali Mahakama ya Kadhi siyo na maslahi na waislamu. Iwapo taarifa mazungumzo kati ya pande mbili- ule wa waislamu na ule wa serikali yatakuwa imekidhi mapendekezo yetu, hapo tutaendelea na mchakato uliopo. Iwapo hayakukidhi mapendekezo yetu, tunapaswa kueleza wazi msimamo wetu ni kutokukubaliana na kinachoendelea na kuueleza ummah ili tusiwe sehemu ya mkakati wa kuleta Mahakama ya Kadhi ambayo siyo ile tunayoitaka.

 

Mapendekezo yetu yalikuwa ni;-

 

  1. Mahakama ya Kadhi wepo katika katiba ya nchi kama ilivyo katika nchi nyingine za Kisekula hata Zanzibar pia.

 

  1. Mahakama ya Kadhi iwekwe katika mfumo wa sheria za nchi kama ilivyo Mahakama ya biashara, ardhi, nyumba n.k. kwa kutungiwa sheria bungeni.

 

  1. Hukumu ya Kadhi iwe ndiyo ya mwisho na kesi iliyohukumiwa na Kadhi isikatiwe rufaa kwenda Mahakama ya kiserikali.

 

  1. Mahakama ya Kadhi igharimiwe na bajeti ya serikali kama ilivyokuwa hapo awali na kama zinavyogharimiwa Mahakama nyingine za kisekta.

 

  1. Waislamu wenyewe ndio waongoze mchakato wa jinsi ya kuiunda Mahakama hiyo na upatikanaji wa Makadhi wenye sifa na vigezo vinavyostahiki na wenye kukubalika katika jamii ya waislamu.

 

 

Baada ya kuyasema hayo, sasa tunatoa tamko letu kama ifuatavyo;-

ÉOó¡Î0 «!$# Ç`»uH÷q§9$# ÉOŠÏm§9$#

TAMKO LA WAISLAMU MINTARAFU KAULI YA CHAMA CHA MAPINDUZI NA SERIKALI JUU YA MAHAKAMA YA KADHI

Tumepokea kauli za viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi Makamu Mwenyekiti wa CCM Mhe. Pius Msekwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mathias Chikawe kuhusu msimamo wa serikali juu ya Mahakama ya kadhi.

 

Akizungumza kupitia runinga ya Taifa (TBC1) siku ya tarehe 25/Juni/2010,  Mhe. Msekwa alinukuliwa akisema kuwa “Chama cha Mapinduzi kimeliondoa rasmi suala la Mahakama ya Kadhi kutoka katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 kwa sababu kimeridhika na hatua zilizochukuliwa na serikali ya CCM katika kulipatia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi”.

 

Aidha alisikika akisema kwamba eti baadhi ya watu hawakuielewa vizuri ibara iliyozungumzia suala la Mahakama ya Kadhi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 kwani ilitaja “kulipatia ufumbuzi” suala la Mahakama ya Kadhi na siyo kuianzisha Mahakama ya Kadhi.

 

Vile vile alisema kwamba serikali ipo katika mazungumzo na jopo la wataalamu waislamu wakiongozwa na Sheikh Mkuu wa Bakwata kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi na waislamu wenyewe siyo na serikali kwani serikali ilishauriwa na Tume ya Mabadiliko ya Sheria iliyoongozwa na Jaji muislamu kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha Katiba.

 

Naye Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mathias Chikawe, akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni siku ya tarehe 26/Juni/2010   alipokuwa akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake alisikika akisema kwamba “Mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi na waislamu wenyewe unaendelea vizuri na kwamba serikali imetenga fungu katika bajeti ya 2010/11 kwa ajili ya kuanzisha Mahakama hiyo.

 

Aidha utaratibu utakaotumika ni kuzipitia sheria za ndoa, talaka, mirathi na waqfu katika kile kiitwacho “Islamic Law Reinstatement Act” ambapo Waziri wa wizara ya Sheria hutumia madaraka yake kuzikubali sheria hizo au kuzikataa.

 

Siku mbili baadaye, Mufti wa Bakwata akanukuliwa na TBC1 akiwataka waislamu wawe wavumilivu hadi hapo mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi utakapomalizika.

 

Kutokana na mambo yanavyokwenda kuhusu kadhia ya Mahakama ya Kadhi, waislamu tunaona kwamba Mahakama ya Kadhi inayokusudiwa kuanzishwa siyo ile tuliyokuwa tunaidai kwa miaka yote na kuhitimisha madai yetu katika viwanja wa Kidongo Chekundu mwaka juzi na kisha kuyawasilisha madai yetu rasmi serikalini kupitia Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Mathias Chikawe, Spika wa Bunge, Mhe. Pius Msekwa na hata baadhi ya waheshimiwa wabunge.

 

Mwaka jana jopo la masheikh lililokuwa likiongoza kudai urejeshwaji wa Mahakama ya Kadhi liliomba kuonana na waziri wa Katiba na Sheria lakini hadi leo hawajafanikiwa kuonana naye na badala yake zinaonekana juhudi za kuileta Mahakama ya Kadhi kwa mlango wa nyuma.

 

Kwa kuwa mwenendo wa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake umekuwa wa kigeugeu, sisi waislamu tunaopigania kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi nchini Tanzania tunatoa tamko letu kama ifuatavyo;-

 

  1. Suala la Mahakama ya Kadhi limegeuzwa kuwa suala la kutafutia maslahi ya kisiasa wakati hili ni suala linalohusu imani ya Waislamu na lisingepaswa kuhusishwa na siasa za vyama, si chama tawala wala vyama vya upinzani.

 

  1. Chama cha Mapinduzi na Serikali yake vimewahadaa na kuwadharau waislamu kwa kuwaona kuwa watu wasioelewa ibara ya 108 (b) ya ilani ya CCM 2005 ibara iliyowazi kwa lugha ya Kiswahili inayotaja kulipatia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi. Sisi bado tunasisitiza kwamba suala hili litakuwa limepatiwa ufumbuzi pale Mahakama hiyo itakapoundwa kwa jinsi tutakavyo waislamu.

 

  1. Mahakama ya Kadhi inayotaka kuundwa siyo ile waislamu waliyokuwa wakiidai kwa miaka mingi sasa kwani sisi tuliitaka serikali kuitambua rasmi Mahakama ya Kadhi kwa kuirejesha kama ilivyokuwa kabla ya kuondolewa kwake kinyume cha katiba mwaka 1963.

 

  1. Inaonekana tayari serikali imeshajipanga kuileta Mahakama ya Kadhi itakavyo yenyewe. Sisi waislamu tuliokusanyika katika viwanja vya Kidongo Chekundu mwezi Oktoba mwaka 2008 hatutoitambua wala kuikubali Mahakama hiyo kwani haitokuwa na maslahi na waislamu wote wa Tanzania.

 

  1. Tunaitaka serikali, kama ina dhamiri ya kweli kuirejesha Mahakama ya Kadhi iliyoporwa mwaka 1963, isishughulike kuiweka au kuitoa Mahakama ya Kadhi katika ilani ya chama chake bali iwakabili waislamu kupitia uwakilishi wa kweli wa jumuiya na taasisi zao kama ulivyoainishwa katika kabrasha lililowasilishwa serikalini badala ya kuipora haki ya waislamu kupitia mgongo wa Bakwata.

 

  1. Iwapo serikali ya CCM haitofanya hivyo kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, basi waislamu hatutokuwa tayari kumpigia kura mgombea wa chama chochote kile aliyeshiriki kuwahadaa waislamu kuhusu Mahakama ya Kadhi.

 

  1. Tunaitaka serikali iache kufanya kazi kwa shinikizo la Maaskofu kwa kukataa kuiweka Mahakama ya Kadhi katika utaratibu wa Mahakama zinazotambuliwa kisheria. Hivi sasa Maaskofu wanaipongeza serikali kwa kutekeleza kauli zao walizozitoa mwaka 2008 kupinga kuanzishwa kwa Mahakama ya kadhi Tanzania.

 

  1. Tunaitahadharisha serikali kwamba iwapo kweli waislamu wataitikia wito wa kuwa na Mahakama za Kadhi nje ya utaratibu unaotambuliwa na mfumo wa sheria za nchi kama inavyotaka, kuna uwezekano kuanzishwa Mahakama za Kadhi kwa staili ambayo itapelekea Mahakama hizo kutoa hukumu hata za makosa ya jinai kama zilivyo nchini Somalia.

 

  1. Tunatoa onyo kwa vyama vya siasa nchini kuacha mara moja kuchezea masuala ya ibada na imani za waislamu kwa kuziweka katika sera na ilani zao za uchaguzi kwa kuweka kisha wasitekeleze. Kufanya hivyo ni kuzicheza shere ibada za waislamu na hilo kamwe halikubaliki kwa waislamu. Tabia hii itapelekea kuja kutiwa sala, swaumu, hija n.k katika sera na ilani zao za uchaguzi.

 

  1. Tunapinga kwa nguvu zote juhudi zozote zile za kuleta Mahakama ya kadhi kupitia mgongo wa Bakwata au taasisi yoyote nyingine ya waislamu bila ridhaa ya pamoja ya waislamu kupitia uwakilishi wa kweli wa taasisi na jumuiya zao huru, Bakwata ikiwemo. Hivi sasa uwakilishi huo haupo.

 

  1. Waislamu wa Tanzania ni sehemu ya waislamu duniani. Mahakama ya Kadhi ni moja ya haki zao za kiimani na kikatiba. Kama kweli katiba ya nchi inaruhusu uhuru wa kuabudu, basi serikali iwape haki kuitekelza waislamu ibada hii bila masharti yoyote kama ifanyavyo kwa ibada ya hijja.

 

WABILLAAHI T-TAWFIIQ

Leave a comment