HEKIMA YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W), KUOA WAKE ZAIDI YA WANNE

 

Bismillaahir Rahmaanir Rahiym

Awali ya yote,napenda kumshukuru Allah(subhaanahu wataala),kwa kuniumba mwanaadamu na kunijaalia kuwa Muislamu.Hii ni neema kubwa kwangu na kwa Waislamu wote.Namshukuru pia kwa kunijaalia afya ya mwili na akili,nikiamini kuwa afya ni miongoni mwa “hasanatu dun-ya”(mema ya dunia).

Rehma na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam),pamoja na Aali na Sahaba zake wote.

Utangulizi

Ndugu zangu waislamu.

Zipo tuhuma mbalimbali kutoka kwa wasio kuwa waislamu,dhidi ya Uislam,Qur an na Mtume Muhammad(sallallaahu alyhi wasallam). Tuhuma hizo na nyinginezo,hazikuanza leo wala jana.Ukisoma historia ya Uislam tokea wakati wa Mtume,bila shaka utakubaliana nami,kuwa : makafiri wa Makka walizua mengi dhidi ya Qur an na Mtume.Wapo waliodai: Qur an, ni ngano na hadithi za kale,ni uchawi wenye kuathiri. Na wengine walisema: Mtume Muhammad ni mshairi(msanii), mchawi, mwendawazimu n.k.

Lengo la tuhuma hizo ni:-

 • Kujaribu kuuchafua Uislam,Qur-an na Mtume Muhammad.
 • Kuwatia hofu wanadaamu.
 • Kulinda na kutetea dhulma zinazofanyika katika ulimwengu, n.k.

Alhamdulillaah,hayakufanikiwa malengo hayo,na Uislamu umebaki kuwa dini pekee ulimwenguni,yenye uwezo wa kujibu na kubomoa hoja potofu zinazo elekezwa dhidi yake kutoka kwa wenye kueneza chuki.

Makafiri wa sasa wana mbinu na mikakati mbalimbali ya kimantiki,kifalsafa na kisheria -za kitwaaghuuti- wanazozitumia katika kuupiga vita Uislamu.Kwa wenye ufinyu wa elimu na uelewa wa dini ya kiislamu,ni rahisi sana kukubaliana na kile kinachoelezwa dhidi ya Uislamu.Eneo muhimu waliloelekeza nguvu na juhudi za opotoshaji wao huo,ni Qur-an na Mtume Muhammad na khasa maisha yake ya ndoa.

 • Kwanini Muhammad alikiuka sheria aliyokuja nayo?Sheria hairuhusu kuoa wake zaidi ya wanne,yeye alioa wake zaidi ya wanne!
 • Muhammad alimuoa Aisha msichana mdogo chini ya miaka saba,huu si ubakaji? Na
 • Aliwezaje kumuoa Zainabu binti Jahshi,aliyekuwa mke wa mtoto wake wa kupanga Zaid bin Haaritha ?

Hayo ni baadhi ya maswali yanayotumiwa na makafiri wa sasa,kumchafua Mtume Muhammad katika ulimwengu wa sasa.

Eneo hili ndilo khasa kiini cha mada yetu.Ni kwa nini mtume Muhammad alioa wake zaidi ya wanne?Sababu zipi zilizokuwa nyuma ya ndoa za Mtume Muhammad?

Hekima ya Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam), kuoa wanawake

Wanachuoni wa kiislamu, wameelezea sababu na hekima nyingi zilizomsukuma Mtume Muhammad kuoa wake zaidi ya wanne,kwa ufupi nizitaje nne, kama ifuatavyo:-

 1. Hikmatut Taalimiyyah.
 2. Hikmatut Tashri’iyyah.
 3. Hikmatul Ijtimaai’yyah.na
 4. Hikmatus Siyaasiyya.
 1. Hikmatut taalimiyyah(hekima ya kielimu).

Bila shaka,lilikuwa lengo la msingi la mtume Muhammad kuoa wake ni; kutoa sehemu ya walimu wa wanawake wa kiislamu,watakao wafundisha Ahkaamu shari’ia(hukmu za kisheria),na mambo mengine yanayokhusu Uislamu wa.Wanawake ni sehemu ya jamii,na wamefaradhishiwa yaliyo ya lazima sawa na walivyo faradhishiwa wanaume.Kwa mantiki hiyo basi,wanawake wengi waliona haya kumuuliza Mtume baadhi ya mambo ya kisheria na khasa yanayowakhusu,kama vile hukmu za hedhi,nifasi,janaba na mambo ya ndoa.Na alikuwa mwanamke akizidiwa na haya anapotaka kumuuliza Mtume baadhi ya mas-ala haya.

Kama ambavyo pia, miongoni mwa tabia za Mtume ni ukamilifu wa haya.Vinasimulia vitabu vya hadith;alikuwa Mtume ni mwenye haya kuliko msichana kigoli(mwanamwali).Haikuwa rahisi kwa Mtume, kujibu baadhi ya maswali anayoulizwa kwa uwazi -unaokidhi haja ya muulizaji- yanayogusa upande wa wanawake.Wakati mwingine akitumia mafumbo,hali iliyopelekea mwanamke kutofahamu nini kusudio la Mtume.

Anasimulia bi Aisha(radhiya llaahu anha),kuwa:

Mwanamke wa kiansar,alimuuliza Mtume kuhusu kuoga hedhi.Mtume akamuelekeza namna ya kuoga,kisha akamwambia;(chukua kipande cha pamba,chenye manukato,jisafishe kwacho)akasema-mwanamke-:Nijisafishe vipi ee Mtume wa Mwenyezi Mungu?Mtume akamjibu:(jisafiche kwacho),akauliza tena:nijisafishe vipi yaa rasuulallaa?Mtume akasema:(subhaanallaah,jisafishe kwacho)!!

Bi A’isha anasema: “nikamvuta pembeni,nikamwambia kiweke sehemu kadha na kadha na fuatishia athari ya damu”.Akamfanunulia kwa uwazi,namna na sehemu anayopaswa kuweka pamba hiyo.

Utaona namna Mtume alivyoona haya kumfahamisha mwanamke huyu kwa uwazi eneo na namna ya kujisafisha.

Aidha walikuwepo wanawake wachache pia,walioweza kuzishinda nafsi zao na haya,wakamuuliza Mtume waziwazi kuhusu yanayowatokea.Tuchukue mfano wa hilo,wa hadithi ya Ummu Salama(mke wa Mtume),anasema:

Alikuja Ummu Sulaym (mke wa abuu Talha),kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu,akasema: ewe Mtume, hakika Mwenyezi Mungu haoni haya katika jambo la haki,je ni wajibu kwa mwanamke kuoga(janaba)akijiotelea?Mtume akamwambia: (ndiyo, atakapoona maji !).Ummu Salama,akasema: “hakika wamefedheheka wanawake,hivi na wanawake hutokwa maji”? Mtume akamjibu,kwa kusema:(ikiwa si hivyo,unadhani- ni kwa sababu gani mtoto hufana na mama yake?)

Kusudio lake Mtume ni kuwa: huzaliwa mtoto kutokana na maji ya mwanaume na mwanamke,na kwa ajili hii hutokea mtoto kufanana na mamake.

Ni kama alivyoseama Allaah(subhaanahu wataala)katika suratul Insaan/2:

إِنَّا خَلَقْنَا الإِنسَانَ مِنْ نُطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعاً بَصِيراً

Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona.

Ibn Abbaas anasema; “yaani maji ya mwanaume na mwanamke yakikutana na kuchanganyika katika mfuko wa uzazi wa mwanamke”.

Naam, mfano wa maswali haya na mengine, alikuwa Mtume akiyaelekeza kwa wakeze baada ya kuoa.Na kwa ajili hii,anasema bi Aysha(radhiyallaahu anha):

Mwenyezi Mungu awarehemu wanawake wa kiansar, haikuwazuia haya kuifahamu dini

Alikuwa mwanamke akienda kwa bi Aysha katika giza,ili amuulize kuhusu baadhi ya mambo ya dini na hukumu ya hedhi,nifaas na janaba,na mengineyo.

Pia inafahamika kwamba,sunna si kauli tu za Mtume,bali imegusa kauli,matendo na yaliyo fanyika mbele yake na akakaa kimya.Yote hayo, ni miongoni mwa mambo ya kisheria ambayo umma wake unapaswa kuyatambua na kuyafuata.Ni nani basi anayeweza kutueleza khabari na matendo yake ya nyumbani tofauti na wakeze,ambao Allaah amewakirimu, wakawa ni mama wa waislamu na wakeze Mtume dunianu na akhera?

Hakuna shaka,wakeze Mtume(radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao),wana fadhila kubwa kwa kunakili hali na matendo ya nyumbani ya Mtume.

Hakika wengi walikuwa ni waalimu na wataalamu wa hadithi, wamefikisha muongozo wake Mtume(alayhi salaam) kwa Masahaba, na wamekuwa mashuhuri kwa uwezo wao mkubwa wa akili na kuhifadhi.

2.  Hikmatut Tashrii’yyah.(hekima ya kisheria).

Tuzungumzie hekima hii,ambayo ni sehemu ya hekima za Mtume kuoa wanawake wengi.

Hekima hii, ilikuwa ni kuvunja na kubatilisha baadhi ya mila na sheria mbovu za kijaahili.Nitoe mfano wa mila ya kujipanga kwa mtoto.Mila ambayo walikuwa Waarabu wakiidumisha kabla ya Uislam(ujio wa Mtume Muhammad).Ulikuwa ni mfumo wenye kurithika baina yao,mtu akimpanga mtoto ambaye si wake na kumfanya sawa na mwanawe wa kuzaa, katika haki zote; mirathi,ndoa,talaka, kuharamisha yote yanayoharamishwa katika nasabu na mengineyo.Mmoja wao akimpanga mtoto,humwambia:”wewe ni mwanangu,nitakurithi na utanirithi”.

Uislamu kwa upande wake,haukukubaliana na batili hii,na haukutaka kuwaacha wakihangaika katika giza la ujinga huu.Hivyo ukaandaa utaratibu mapema,kwa kumpa ilham(msukumo wa kufanya jambo) Mtume Muhammad,ampange mtoto -ilikuwa kabla hajapewa utume- ,akampanga Zaid ibn Haaritha,kama ilivyokuwa ada ya waarabu.

Na sababu ya Mtume(alayhi salaam),kumpanga Zaid kuwa mwanawe,ni kisa katika visa vyenye kupendeza,na  simulizi nzuri yenye kusisimua.Wamesimulia wafasiri na watu wa sira. Nikupe kwa urefu wake ili uende sambamba nami katika hekima hii:-

Haaritha ibn Sharaahiyl(babake Zaid),aliandaa safari ya mkewe Sa’adaa,kwenda kuwatembelea wazazi wake wa bani mui’n. Akatoka kumsindikiza mkewe,mikononi akiwa kambeba mtoto wao mdogo wa miaka minane Zaid ibn Haarith.Kila alipokusudia kuaga msafara huu,ili arudi nyumbani na kuendelea na kazi zake,anapata huruma na huzuni.Lakini hatimaye shaka na wasiwasi vikamtoka na msafara ukaanza safari. Haarith akimuaga mwanawe na mama yake hali machozi yakimtiririka! Akasimama kwa muda mrefu alipokuwa kasimama, mpaka msafara ukatoweka machoni mwake, akahisi moyo wake haujarudi sehemu yake umesafiri pamoja nao.

Sa’adaa(mamake Zaid),kakaa kwa wazazi wake muda aliyopenda Mwenyezi mungu akae.Ghafla mji wao ukavamiwa na makabila dhalimu,wakashindwa vita banu mui’n. Miongoni mwa mateka waliyochukuliwa ni Zaid ibn Haaritha.Akarejea mama yakeke Zaid pekee bila mwanawe.Na hakumaliza kumsimulia mumewe juu ya kilichotokea, ila Haaritha akianguka na kuzirai!!

Haaritha akabeba fimbo yake begani,akipita miji na kuvuka majangwa,akiuliza makabila na misafara kuhusu mwanawe bila mafanikio.Akiiliwaza nafsi huku akiongoza farasi wake,kwa kusema:

Nalia juu ya Zaid mwanangu                                     ilhali sijui alichotendwa

Je yuhai niwe na matumaini                                      au kesha fikwa na mauti

Wallaahi mie sijui                                                            lakini ntaendelea kuuliza

Hunikumbusha  Zaid kila                                              jua lichomozapo na lizamapo

Na uvumapo upepo                                                        husisimua utajo wake

Urefu ulioje wa huzni yangu                                     urefu ulioje wa woga wangu


Kabila likachukua mateka moja kwa moja mpaka Makka katika soko la U’kaadh,lililokuwa gulio kubwa wakati huo, na kuwauza mateka. Zaid akangukia mikononi mwa Hakiim ibn Hizaam,baada ya kumnunua akamzawadia shangazi yake Khadija bint Khuwaylid mke wa Mtume Muhammad(alayhi salaam).Wakati huo ni Muhammad na si nabii,bado wahyi haujateremka kwake,pamoja na sifa zote zinazostahiki yeye kuwa nabii.Khadija akamzawadia Muhammad mumewe,mtumishi wake(Zaid),akampokea kwa furaha na kisha akamwacha huru,akimfanyia huruma na upole kwa moyo wake wote!

Ukafika msimu Hijja,watu wa mji wa Zaid wakakutana naye Makka,wakamfikishia mateso na huzuni za baba yake.Zaid akawapa salamu,mapenzi na shauku aliyonayo kwa baba na mama yake,na akawaambia:”mwambieni baba asiwe na khofu,mimi huku nimepata mzazi bora”!

Haarith alipopata taarifa za alipo mwanawe,akafunga safari yeye pamoja na nduguye Ka’abu mpaka Makka.Walipofika wakamuulizia Muhammad Al-amiin(kama alivyokuwa akijulikana),na walipokutana na naye,wakamwambia:”ewe ibn Khataab,enyi watu wa Haram(Makka),watu msaidiao wenye shida na mlishao watumwa;tumepata taarifa mwanetu yupo kwako,na tumesikia pia uzuri wa tabia yako.Lakini wewe unajua nafasi ya mtoto ndani ya moyo wa mzazi,tunakuomba utusaidie kwa kutupa mwanetu, nasi tuko tayari kukupa fidia ya chochote utakacho“! Mtume(s.a.w)anajua mapenzi ya Zaid kwake,na wakati huo anapima haki ya mzazi kwa mwanawe.Akawaambia:(tumpeni  Zaid nafasi ya kuchagua,akikuchagueni nyinyi sintahitaji kutoka kwenu chochote,na akinichagua mimi,basi wallaahi siwezi kuchagua fidia kuliko yule aliyenichagua).Ukameremeta uso wa Haaritha kwa furaha,na akasema:”umetufanyia uadilifu kwa (kumlea mtoto) na umetuzidishia uadilifu(kwa kutohitaji fidia).Akaitwa Zaid kisha Mtume akamuuliza:(unawajua hawa ni akina nani ewe Zaidi?)Akajibu:”ndiyo! huyu ni baba yangu na huyu ni a’mi yangu”. Mtume akamuuliza:(ni yupi kati yao na mimi unayemchagu?)Zaid akainua kichwa akamtazama baba yake na a’mi yake, yakambubujika machozi,akasema maneno yenye kusisimua:”siwezi kumchagua yeyote juu yako,wewe ni baba na a’mi”!!  Yakabubujika macho ya Mtume machozi  ya shukurani na mapenzi,kisha akamshika Zaid mkono, akatoka naye mpaka kwenye uwanja wa Al-ka’aba walipokuwa Makureyshi wameketi, na akanadi:(shuhudieni enyi makureyshi,kuwa;Zaid ni mwanangu, nitamrithi na atanirithi…) Moyo wa Haaritha ukakaribia kupasuka kwa furaha;mwanawe si tu anahesabika kuwa huru kama alivyozaliwa,bali ni mtoto wa mtu ambaye Makurayshi wanamwita “aswaadiqul amiin” (mkweli na muaminifu),mtoto wa banu Haashim,ukoo wenye kuheshimika Makka nzima.Haaritha  akarejea yeye na nduguye,mioyoni mwao wakiwa na utulivu juu ya mtoto wao,kwani wamemuacha kwa bwana wa Makka.

Anasimulia bukhari na muslim,kwa hadithi ya Abdillaahi ibn Umar(radhiyallaahu anhuma),anasema:

((Hakika Zaid ibn Haarith,kipenzi cha Mtume,Hatukumwita ila Zaid ibn Muhammad.mpaka ilipoteremka Qur-an:(…..Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu…….) Basi Mtume akasema:(wewe ni Zaid ibn Haaritha ibn Sharaahiyl).

Turudi katika nukta yetu.

Mtume Muhammad(alayhi salaam),alimuozesha Zaid binti wa shangazi yake Zainabu bint Jahshi Al-asadiyya.Lakini ndoa yao haikuchukua muda mrefu,kutokana na uhusiano mbaya baina yao.Zainabu akimtolea Zaid maneno makali,kwa kujiona yeye ni bora kuliko Zaid,kwa sababu,akimuona Zaid ni mtumwa asiyejulikana familiya wala ukoo wake pale Makka.

Kwa hekima aliyokusudia Mwenyezi Mungu;Zaid akamtaliki mkewe. Allah akumuamrisha Mtume Muhammad amuoe Zainab,ili kuvunja mila ya kutomuoa aliyekuwa mke wa mtoto wa kupanga.Lakini Mtume Muhammad akakhofia ndimi za makafiri na wanafiki,wasijesema:’Muhammad kamuoa mke wa mtoto wake”.Akasita kutekeleza amri hii(ya kumuoa Zainab),mpaka alipolaumiwa na Allaah(subhaanahu wataala),kwa kitendo hicho:

وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّهُ أَحَقُّ أَنْ تَخْشَاهُ فَلَمَّا قَضَى زَيْدٌ مِنْهَا وَطَراً زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَراً وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولاً

33|37 ………nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t’alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa )).

Sheria hii ya kutooa mke wa mtoto wa kupanga baada ya kumuuacha, ilimalizika rasmi baada ya Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam) kumuoa Zainabu bint Jahshi,na Allaah akateremsha aya, kusisitiza alichokifanya Mtume uhalali wake na kuvunja hoja za makafiri na wanafiki waliohoji kwanini Muhammad amuoe mke wa Zaid?Anasema Allaah katika Qur-an:

مَا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِنْ رِجَالِكُمْ وَلَكِنْ رَسُولَ اللَّهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيماً

33|40|Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.))

Hivyo basi,ndoa hii ya Mtume Muhammad(alayhi salaam) na Zainab,ilikuwa ni kwa Amri ya Mwenyezi Mungu,na haikuwa kwa sababu ya kukidhi matamanio ya mwili,kama wanavyodai baadhi ya makafiri na maadui wa Uislam.Ilikuwa ni kwa lengo na makusudio makhsusi,kuvunja sheria na mila za kijahili,na amelielezea wazi Mwenyezi Mungu lengo hilo  na kwa ufasaha mkubwa,aliposema:

زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَراً ……

……….tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t’alaka…….))

Hakika alitawalia Mwenyezi Mungu kumuoza nabii wake Zainab,mke wa mtoto wake wa kupanga.Na kwa sababu hii,Zainab akijifakharisha kwa wakeze  wa Mtume.

Anasimulia Bukhaar ya kuwa:

((“Alikuwa Zainab akijifakharisha kwa wakeze Mtume,akisema:”wamekuozesheni familia zenu,nami amenioza Allaah kutoka juu ya mbingu ya saba”.))

Hivyo ndivyo ilivyokuwa ndoa hii,kwa sababu ya kuweka sheria mpya,inayoruhusu kuoa wake wa watoto wa kupanga,baada ya kuachika,na isiwe tabu tena kwa waislamu kuwaoa kwa kigezo hicho.

3.  Hikmatul ijtimaai’yya.(hekima ya mahusiano ya kijamii).

Ama hekima hii, inadhihirika kwa uwazi kabisa,kwa Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam),kumuoa bint ya Abu bakri siddiq(radhiyallaahu anhu),na kumuoa bint ya  U’mar ibn Khattaab(radhiyallaahu anhu).Kisha kutafuta uhusiano wa kuoleana na Makureysh, kwa kuoa wanawake miongoni mwao.Kitu kilichopelekea uhusiano  madhubuti kati ya familiya na makabila ya kikureishi,na kugeuza nyoyo zao kwake.

Mtume alimuoa bi A’isha binti wa aliyekuwa kipenzi na mwenye thamani zaidi kwake. Naye si mwengine ila ni Abu bakri siddiyq, ambaye ni miongoni mwa waislamu wa mwanzo katika Uislam,aliyetoa mali,nafsi na roho yake kwa sababu ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.Aliyevumilia aina mbalimbali za adha katika kuupigania Uislamu,mpaka Mtume Muhammad akasema kuelezea ubora wake:

(( Hakuna yeyote aliyetoa msaada kwetu,ila tumemlipa kwao,ispokuwa Abu bakr,msaada wake kwetu atamlipa Allah siku ya kiyama.Haikunifaa mali ya yeyote kabisa,kama ilivyonifaa mali ya Abu bakr.Sikumfikishia yeyote Uislamu ila alisita,ispokuwa Abu bakr hakurudi nyuma.Na lau ningekuwa na uwezo wa kumfanya mtu khaliyl(kipenzi),hakika ningemfanya Abu bakri kuwa khaliyl.Fahamuni kuwa; sahibu yenu ni khalili wa Mwenyezi Mungu mtukufu!)).

Kwa maana hiyo,Mtume hakuona malipo ya Abu bakri katika dunia hii,zaidi ya kuburidisha macho yake kwa ndoa hii ya bint yake,na uwepo kati yao ukwe na udugu,utakao zidisha urafiki na uhusianao wao madhubuti.

Kama alivyo muoa bi Hafsat bin U’mar,ilikuwa ni kumsatarehesha U’mar kwa; Uislam, imani ya kweli, ikhlasi na kupambana kwake katika dini hii.U’mar ndiye shujaa wa Uislamu,ambaye Mwenyezi aliuupa nguvu Uislam na Waislamu kwa sababu yake, na kuiinua bendera ya dini.Ukawa uhusiano kati ya Mtume na U’mar kwa njia hii ya kuoa binti yake, ni malipo bora, kwa kujitolea kwake katika dini ya Uislamu.

Hiki ni kisa kifupi cha Hafsa mpaka kuolewa na Mtume:

Hafsa bint U’mar(radhiyallahu anhuma),alizaliwa  miaka mitano (5) kabla ya Mtume kupewa utume.Alikuwa mke mwema wa sahaba Khunays ibn Hadhaafa assahmiy,ambaye alikuwa ni miongoni mwa masahaba waliohama mara mbili.Alihama mara ya kwanza kwenda Habasha (Ethiopia),kisha Madina kumnusuru Mtume(alayhi salaam).Khunays alihudhuria vita vya Badr,kisha Uhud.Akafa kutokana na majeraha aliyoyapata katika vita Uhud,akimuacha mkewe Hafsa nyuma yake akikaa eda , hali yakuwa ni binti mwenye umri wa miaka ishirini na tano(25).

Mtume kumuoa Hafsa

U’mar,alipata uchungu na maumivu kwa binti yake kuondokewa na mumewe,akiumia zaidi kwa kumuona bado ni binti mdogo katika upweke wa gereza kumbwa la ujane.Binti ambaye alikuwa akineemeka kwa kufurahia ya maisha ya ndoa. Akaanza kufikiria; ni nani atakayekuwa mume wa binti yake, baada ya kumalizika eda?Siku zikapita mfululizo,hakuna aliyejitokeza kumposa,naye hajui kuwa,tayari Mtume kaonesha nia ya kumuoa na kampa siri hiyo Abu bakri .Muda ulipokuwa mrefu,binti yake akiwa katika machungu ya ujane,akamtangazia Abu bakr amuoe.Abu bakri hakumjibu chochote. Hakukata tamaa akamfuata U’thmaan ibn A’ffaan,akimtaka amuoe Hafsa.U’thmaan akamjibu:”sihitaji kuoa kwa sasa”! U’mar akawakasirikia,na akalalamika kwa Mtume,kuhusu ahali aliyonayo kwa binti yake.Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam),akamwambia:((atamuoa Hafsa -mwanaume-bora kuliko U’thmaan,na ataolewa na U’thmaan -mwanamke- bora kuliko Hafsa)).Mtume akamuozesha Uthmaan binti yake Ummu Kulthuum,baada ya kifo cha dada yake Ruqqayya binti Rasuul. Baada ya Mtume kumuoa Hafsa,Abu bakri akakutana na U’mar,akatoa udhuru na kusema:”Usinikasirkie ewe U’mar,nilimsikia Mtume akimtaja Hafsa,nisingeweza kutoa siri ya Mtume, na kama Mtume angemuacha basi ningemuoa”.

Kadhalika, katika kutumia ndoa kama sehemu muhimu ya kuimarisha mahusiano na sahaba zake, Mtume aliwaoza mabinti zake wawili(Ruqqayya na Ummu kulthuum) kwa  U’thmaan ibn A’ffaan, na Fatma kwa  A’liy ibn abiy Twaalib.

4.  Hikmatus siyaasiyyat(hekima ya kisiasa).

Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam) alioa baadhi ya wanawake,kwa ajili ya kuziunganisha nyoyo kwake,na kuyavuta makabila upande wake.Inafahamika kuwa,mwanadamu anapooa katika kabila au familiya yoyote ile,hupatikana uhusiano wa udugu,utakaotoa msaada, nusra na ulinzi kwa aliyeoa ndani ya kabila au familiya hiyo.Na hiyo ndiyo tabia ya ndoa.

Tuchukue baadhi ya mifanoya hilo,ili iwe wazi hekima hii:-

1. Mtume alimuoa bi Juwayriyya bint Al-haarith,kutoka banu mustwalaq. Juwayriyya,alikuwa ametekwa yeye, qaumu na familiya yake.Baada ya kuingia katika mateka,akataka kujikomboaAkaja kwa Mtume ili apate msaada wa mali,ajikomboe kutoka mikononi mwa Waislamu.Mtume akamuekea wazi;amtolee fidia na amuoe,akakubali hilo kisha Mtume akamuoa. Masahaba walipoona hivyo,wakasema: “wakweze Mtume wawe mikononi mwetu(haiwezekani),Masahaba wakawaacha huru wote.Banu mustalaq walipoona wema,utu na heshima hii waliyopewa,wakasilimu wote na wakaingia katika dini ya Allah,na wakawa waumini wazuri wa dini hii.

Ndoa hii ya Juwayriyya,ikawa ni baraka kwake,qaumu na familiya yake kwa ujumla.Kwa kuwa ilikuwa ni sababu ya kuachiwa huru na kusilimu kwao.

2. Kadhaalika,Mtume alimuoa bi Safiyya bint Huyyay ibn Akhtab,ambaye alitekwa baada ya kufa mumewe katika vita vya Khaybari na akaingia katika mgao wa baadhi ya Masahaba.Watu wa rai na shuura,wakasema: “Safiyya ni bi mkubwa (anayeheshimika) wa banu Quraydha(mayahudi wa Madina),haitakuwa vizuri kuwa chini ya mtu,ila kwa Mtume”.Wakamueleza Mtume juu ya ushauri huu.Mtume akamwita Safiyya na kumwambia achague kati ya mambo mawili:-

a) Ama amuache huru,kisha amuoe awe mkewe,au

b) Amuache huru na arudi kwao.

Juwayriyya akachagua kuachwa huru kisha aolewe na Mtume.Alikubali kuolewa na Mtume,baada ya kuona hadhi,utukufu na muamala mzuri wa Mtume Muhammad(alayhi salaam).Akasilimu na wakasilimu idadi kubwa ya ukoo wake.

Inasimuliwa kuwa:

(( Safiyya alipoingia kwa Mtume, Mtume akamwambia:<<Hakuacha baba yako kuwa ni adui yangu mkubwa mpaka alipouawa na Mwenyezi Mungu>>,Safiyya akasema: “hakika Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake:”wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine“.Mtume akamwambia:<<chagua: ukichagua Uislamu nitakuchukua mwenyewe,na ukichagua uyahudi hakika nitakuacha huru na urudi kwa watu wako>>.Akasema: ” Nimeupenda Uislamu,na nimekuamini kabla hujaniita katika dini yako.Na sina haja ya uyahudi,na katika uyahudi sina mzazi wala ndugu.Umenipa khiyari kati ya ukafiri na Uislamu,basi Allah na Mtume wake nawapenda zaidi ya kuachwa huru na kurudi kwetu”)). Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam),akamuoa.

3. Pia Mtume Muhammad alimuoa Ummu Habiba(Ramla bint abu Sufiyaan),ambaye -abu Sufyaan- alikuwa kwa wakati huo amebeba bendera ya Ushirikina,na adui mkubwa wa Mtume.Alisilimu ummu Habiba katika mji wa Makka,kisha akahamia Habasha pamoja na mumewe(U’baydullaahi ibn Jahsh) akikimbiza dini yake.Huko akafa mumewe -baada ya kuritad na kuingia katika unasara-,na akabaki mpweke ,yeye na mtoto yatima(Habiba).Baada ya Mtume kupata taarifa hizo,akatuma ujumbe kwa Abraha(mfalme wa habasha)amuoze. Kwa sababu,kama ummu Habiba angerejea kwa baba yake au familia yake; wangemlazimisha ukafiri au kumuadhibu adhabu kubwa.

Abraha alipopata ujumbe huu akafurahi sana,hakuna ajuaye kipimo cha furaha hiyo ila Allah(subhaanahu wataala). Akatoa dinaari mia nne(400) za mahari kwa niaba ya Mtume Muhammad,pamoja na zawadi zenye thamani kubwa.Ummu Habiba alipofika Madina,akaolewa na Mtume Muhammd(sallaallaahu alayhi wasallam).

Zilipomfikia abuu Sufyaan khabari za ndoa hii,akaikubali na kusema:’Hilo ni dume lisiloguswa pua yake”.Akajifakhari kwa Mtume na haukipanga chochote kwa Mtume mpaka Mwenyezi Mungu ilipomwongoza katika Uislamu.

Hapa tunapata picha ya hekima ya Mtume kumuoa binti wa abu Sufyaan; ndoa hii ilikuwa sababu ya kupunguza adha kwake Mtume na kwa Sahaba zake,khasa baada ya kuwepo uhusiano huu wa kuoleana na nasabu.Pamoja na kuwa abuu Sufyaan wakati huo, ndiye aliyekuwa adui mkubwa katika banu Umaaya kwa Mtume na Waislam.Ikawa ndoa hii ni sababu ya kuutia mapenzi moyo wa abu Sufiyaani na jamaa zake kwa Mtume.Kama ambavyo Mtume alivyomchagua ummu habiba kwa sababu ya kuheshimu imani yake,kwani alikosana na wazazi na jamaa zake, na akahama Makka kuinusuru imani na dini yake.Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na juu ya wakeze  wote wa Mtume Muhammad(sallallaahu alayhi wasallam).

Naam,hizo ni miongoni mwa hekima za Mtume Muhammad kuoa wanawake wengi kuliko idadi waliopewa waislamu.Hakuoa kwa sababu ya kukidhi matamanio ya mwili,bali ni kwa amri ya Allah na hekima makhususi.Na kama ingekuwa nyuma ya ndoa hizi za  Mtume,ni matamanio ya kimwili -kama wanavyodai baadhi ya makafiri-,basi engelioa wanawake mabinti wenye umri mdogo(vigoli), ambao hawajawahi kuolewa na kufiwa na waume zao.Kinyume na wanavyodhani makafiri,Mtume hakuoa mwanamke bikra ila A’isha,na hakuoa mwanamke mwengine ila baada ya kufiwa na bi Khadija, Mtume akiwa na umri wa miaka khamsini(50).Maana yake,Mtume aliishi na bi Khadija miaka  ishirini na tano(25),mwanamke aliyemzidi miaka kumi na tano(15),aliyeolewa na wanaume wawili kabla yake;hakutamani wala kuhitaji mke mwingine katika kipindi chote alichoiishi na bi Khadija.Wala hakuoa idadi hiyo ya wanawake,ila baada ya kufikisha umri zaidi ya miaka khamsini na tano(55),kipindi ambacho vita vimeacha wanawake wakiwa wajane.

Lengo ilikuwa,ni kuelezea hekima za Mtume kuoa wanawake zaidi ya wa nne.Nikusihi uvute subira; naandaa makala -biidhni llaahi- itakayoelezea majina na wasifu wa kila mmoja wa wakeze Mtume Muhammad (sallallaahu alayhi wasallam).

Advertisements

One thought on “HEKIMA YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W), KUOA WAKE ZAIDI YA WANNE

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s