HOTUBA YA MGENI RASMI MAMA SALMA KIKWETE KWA WANAJUMUIYA WA TAMSYA KATIKA MAADHIMISHO YA ”HIJAB DAY”. TAREHE 07 JUNE 2009 KATIKA UKUMBI WA STARLIGHT

Bismillahr Rahmanir Rahiym,

Ndugu Amira wa TAMSYA Taifa,

Ndugu Amira wa TAMSYA mkoa wa Dar essalaam,

Ndugu maamira TAMSYA kutoka wilaya za  Ilala,Kinondoni na Temeke

Ndugu maamira wa TAMSYA  kutoka mashule na vyuo mbalimbali mkoa wa Dare s salaam

Ndugu wanajumuiya wa  TAMSYA  na waislamu wote na wagwni waalikwa mliohudhuria katika ukumbi huu huu,

 Asalaaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuhu

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Allah (S.W) kwa kutuwezesha kuhudhuria katika kongamano hili la kihistoria lililoandaliwa na TAMSYA tuseme Alhamdulilah.

Pia napenda kumtakia rehema na amani Mtume wetu Muhammad (S.A.W)  pamoja na ahli zake na maswahaba zake na wote wema waliotangulia mbele ya haki.  Mwenyezi Mungu awawie radhi Inshaalah.

Kwa heshima na taadhima kwa siku tukufu kama ya leo napenda kuzungumza nanyi kuhusu Masuala mbalimbali yanayo muhusu mabinti na wanawake wa kiislamu katika jamii.

Ndugu zangu waislamu wenzangu,

 Leo ningependa tutizame jinsi uislam unavyo muenzi na kumsitiri mwanamke. Nitafanya haya kwa kutizama hoja zifuatazo:-

Jibu la swali hili litapatikana katika hoja zifuatazo:-

Ndugu mabinti na kina mama wa kiislamu kimaumbile mwanamke na mwanamume asili yao ni moja. Kama tunavyo kumbushwa katika Qur-an sura ya nne aya ya kwanza (4:1) . Nanukuu,

“Enyi watu mcheni mola wenu ambae amekuumbeni katika nafsi (asili) moja (Adam) na akamuumba mkewe katika nafsi ileile,na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutoka katika wawili hao”.

Kwa mujibu wa aya hii iliyomo katika Qur-an tukufu tunajifunza kuwa pamoja na asili moja ya kuumbwa kwetu kila mmoja kati ya mume au mke anamtegemea mwenziwe.

Na katika kutilia mkazo kutegemeana huku Mwenyezi Mungu amesema tena katika Qur- an  sura ya pili aya ya mia moja themanini na saba (2:187) 

Ndugu zangu wanafunzi wa kiislamu kwa kuwa nyinyi ni wasomi mnafursa nzuri ya kusoma kile ambacho Mwenyezi Mungu anakiridhia mbali na kubagua katika elimu. Na ukiisoma Qur- an vizuri utaona hoja nyingi zinadhihirisha kuwa Uislamu haumdhalilishi mwanamke.

Ndugu wanafunzi wa kiislamu hoja nyingine inayodhihirisha kuwa Uislamu haumdhalilishi mwanamke ni kutokana na lengo la kuumbwa wanaume na wanawake hapa ulimwenguni kuwa ni moja . Nalo linapatikana katika sura ya hamsini na moja aya ya hamsini na sita(51:56)  Mwenyezi Mungu anasema, Nanukuu,

“….Sikuwaumba majini na watu ila waniabudu..”

Ndugu wanafunzi wa kiislamu, kumuabudu Allah (S.W)  katika maisha ya kila siku ni kuishi kwa kufuata muongozo wake, kama Mwenyezi Mungu alivyo tuagiza katika Qur an tukufu sura ya nne aya ya mia moja na ishirini na nne(4:124).

Mwenyezi mungu anasema, Nanukuu

“Na watakao fanya vizuri wakiwa wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini basi hao wataingia peponi wala hawata dhulumiwa hata kidogo”.

 

Ndugu wana TAMSYA ifahamike kuwa jukumu la kusaidia maendeleo ya waislamu ni la kila muislamu pasi na kubagua mwanamume au mwanamke

kwani ukiangalia hata katika historia ya uislamu utawaona akina mama wengi walijitokeza katika kuleta maendeleo ya Uislamu.

Ndugu wana jumuiya ya TAMSYA mkumbuke kuwa ,kuwa imara kiuchumi ni sababu moja wapo kubwa ya kumpa mtu hadhi katika jamii yoyote ile.

Jamii nyingi za kale zilimnyonya mwanamke na kumnyima haki za kiuchumi na kumfanya kama mtumwa katika jamii. Wanawake hawakuwa na haki ya kumiliki mali na hawakuwa na haki ya kurithi.

Pamoja na propaganda zilizopo kuwa uislamu una mdhalilisha mwanamke, Uislamu ndiyo uliomuinua mwanamke kiuchumi na kimaadili.

Ndugu wana TAMSYA  katika sheria za kiislamu mwanamke:

(a)     Anayo haki ya kupata mahitajio yake yote ya maisha kama vile

 chakula,mavazi,malazi,makazi n.k kutoka kwa mumewe

(b)     Ni haki yake kupewa mahari na mumewe kabla ya kuolewa na ni haki

yake pekee kumiliki mali hiyo inayotokana na mahari pasi na

kuingiliwa na wazazi wake,walezi wake,mume wake au yeyote yule.

(c)     Vile vile,sheria ya kiislamu imempa mwanamke haki ya kurithi mali ya

wazazi wake,mume wake,watoto wake na jamaa zake wengine wa

karibu kinyume na hali ilivyokuwa kabla yakuja kwa uislamu.

(d)         Vile vile katika sheria ya kiislamu mwanamke amepewa uhuru kamili wa kiuchumi na kumiliki alichokichuma bado ni jukumu la mumewe kumpatia mahitajio yake yote muhimu ya maisha kama vile chakula,mavazi,malazi,n.k

Hebu niwaulize ukiangalia hapa ni kweli mwanamke anadhalilishwa?

Ndugu wana TAMSYA mkumbuke kuwa  pamoja na uislamu kuruhusu mwanamke kujiajiri na kumiliki mali hata hivyo uislamu unaruhusu mwanamke kufanya  kazi yoyote inayo heshimu hadhi ya mwanamke kwa kuchunga mipaka aliyoiweka Allah (S.W).

Ndugu wana TAMSYA ni vizuri tukijikumbusha kuwa katika sheria ya kiislamu mwanamke akiwa mgonjwa uislamu unataka mwanamke huyu achunguzwe ugonjwa wake na muuguzi ama daktari wa jinsia ya kike. Hivyo basi ni wajibu wenu ninyi kama   mabinti kufanya bidii katika masomo ya sayansi ili kukabiliana na changa moto za kuwa na madaktari wachache wanawake.

Nimepata kusikia kuwa baadhi yenu mnafaulu vizuri katika masomo ya sayansi  lakini  mnaamua kujiunga na masomo mengine mkifika Chuo Kikuu, huko ni kujidhulumu na kuwadhulumu binadamu wenzako kwa kuwakosesha huduma ambayo wangeweza kuipata hasa ya tiba pale utakapokuwa daktari.

Baadhi yenu badala ya kujiunga na masomo ya udaktari, mnadai eti Udaktari ni mgumu hizo ni fikra potofu na msikubali kudanganywa,jamii inahitaji madaktari wengi wa kike. Mwanamke anaweza kama awezavyo mwanaume.

Ndugu wana TAMSYA napenda nichukue fursa kuwasisitiza kuwa hata serikali imetoa kipao mbele kwa masomo ya sayansi na kipaombele kimetolewa zaidi kwa wanawake, ni wajibu wenu kufanya bidii ili tuweze kupata madaktari wengi hapo baadae Inshaalah.

 Ndugu wana TAMSYA pamoja na haki za kiuchumi alizopewa mwanamke bado uislamu umempa haki za kijamii  zifuatazo:

Kwanza kabisa, Mwanamke amepewa uhuru kamili wa kuolewa na mwanamume ampendae, mkumbuke kuwa katika ndoa ya Kiislamu ni makosa kumuozesha binti kinyume na ridhaa yake na ni makosa kumkataza binti kuchagua ampendae ila akitaka kuolewa na ambae sheria ya Kiislamu imekataza.

Vile vile wanawake wajane na waliotengana na waume zao wana haki na uhuru kamili kuolewa tena. Haki hii haipatikani katika jamii nyingi ulimwenguni.

Ndugu wana TAMSYA napenda kuchukua fursa hii adhimu kuongea nanyi kidogo kuhusu ELIMU.

Katika uisamu kujielimisha ni faradhi (lazima) kwa waislamu wote wanaume na wanawake. Unaweza ukapata ushahidi wa hili kutoka katika Qur-an sura ya tisini na sita aya ya kwanza(96:1). Mwenyezi mungu anasema, Nanukuu’’

“ Soma kwa jina la mola wako aliyeumba”.

Aya hii na nyinginezo zinahimiza elimu katika uislamu, hazimbagui mwanamke.

Kutokana na tabia ya baadhi ya jamii ulimwenguni  za kuwanyanyasa wanawake na kuwaona kuwa ni nuksi wasiostahiki kulelewa na kuelimishwa UISLAMU umetoa motisha mkubwa wa ahadi ya kupata malipo makubwa kutoka kwa Allah (S.W) kwa kuwalea watoto wa kike vizuri na kuwaelimisha ipasavyo.

Katika hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmad, Mtume (S.A.W) amesema

“Yeyote atakayewalea mabinti wawili hadi wakakua,yeye na mimi siku ya kiyama tutakuwa kama hivi (akaonyesha vidole vyake viwili ili kupiga mfano watakavyokuwa karibu sana huko peponi).

Lengo la mafundisho haya  ya Mtume (S.A.W) ni kuwaondosha watu katika fikra dhaifu za kuwaona watoto wa kike kuwa kama si binadamu.

 Tumeona hapo juu kuwa jamii ya Kiislamu inahitaji madaktari,wauguzi,walimu n.k ni dhahiri kuwa itabidi waelimishwe kwanza ndio waweze kupata ujuzi wa kufanya kazi hizo.

Ndugu akina mama,mabinti na wana jumuiya hii ya TAMSYA nisingependa kumalizia hotuba yangu pasi na kuzungumza nanyi kuhusu umuhimu na  haki ya stara kwa mwanamke.

Mipaka ya stara ya mwanamke kutokana na umbile lake ni tofauti na mipaka ya stara kwa mwanamume.Ama mipaka ya stara kwa mwanamume  ni kati ya kitovu na magoti na stara ya mwanamke ni mwili mzima isipokuwa uso na vitanga vya mikono.

Haya si maneno yangu bali ni ya Mola mtukufu kama alivyo tuamrisha katika kitabu chake kitukufu aliposema kumwambia Mtume (S.A.W. Nanukuu.

“Na waambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao,wala wasidhihirishe viungo vyao ,isipokuwa vinavyo dhihirika (uso na vitanga vya mikono) na waangushe shungi zao(mitandio yao) mpaka vifuani mwao” mwisho wa kunukuu.

Kabla sijatoa maelezo ya aya hiyo tukufu naomba tuangalie aya nyingine iliyomuhimiza mwanamke kujisitiri.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema  katika Qur-an. Nanukuu

“Ewe mtume waambie wake zako na binti zako na wanawake wa kiislamu wajiteremshie uzuri nguo zao.kufanya hivyo kutawapelekea upesi wajulikane(kuwa ni watu wa heshima) wasibughudhiwe(sura ya 33 aya ya 59)

Kwa mujibu wa aya hizo mbili nilizozitaja hapojuu ni wazi kuwa kuna umuhimu mkubwa  kwa mabinti na wanawake wa Kiislamu kujisitiri ili wasibughudhiwe pindipo wapitapo barabrani na endapo  mavazi ya heshima yatavaliwa yatasaidia kuiokoa  jamii na uchafu wa zinaa.

Hata hivyo kwa kuwa bado wapo mabinti wa kiislamu katika shule za msingi,sekondari na vyuo ni jukumu la jumuiya hii tukufu kuendelea kufanya semina,makongamano, HIJAB DAY kama hii ya leo ili kuendelea kuwahimiza nao waweze kujisitiri kama wenzao kwani wengine wanatoka katika familia ambazo elimu ya dini ni ndogo na hawajajua umuhimu wa kujistiri ni jukumu letu sote kuwasaidia ili nao wavae kama nyinyi mlivyovaa kwa kweli mnapendeza sana. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awalinde na vitimbi vya shetani ili muweze kudumu na vazi hili tukufu katika maisha yenu yote Inshaalah.

Napenda kuishukuru kwa mara nyingine Jumuiya hii kwa kuniteua mimi kuwa  mlezi wenu nimefurahi na nawaahidi tutakuwa pamoja, INSHAALAH.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s